VYUO VYA MAENDELEO YA WANANCHI - VMW (FCD’S)
Historia fupi ya Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi
Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (VMW) ni “Taasisi za Kiserikali”
ambazo zilianzishwa mwaka 1975 kutokana na wazo la Baba wa Taifa, Hayati
Mwalimu Julius K. Nyerere, baada ya kutembelea nchi ya Sweden na kuona mfumo wa
elimu isiyokuwa rasmi ulivyokuwa unaendeshwa na taasisi zinazojulikana kama Folk
High Schools.
Vyuo ya Maendeleo ya Wananchi vilianzishwa kama sehemu ya awamu
ya tatu ya Elimu ya Watu Wazima. Hatua ya kwanza ilihusu kuondoa ujinga
wa kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu. Hatua ya pili ilikuwa ya
kuhakikisha kuwa mafanikio yaliyopatikana katika hatua ya kwanza yanakuwa
endelevu na watu hawaurudii ujinga. Hatua ya tatu ilikuwa kuanzisha taasisi
ambazo zingetoa maarifa na stadi kwa wananchi. Aidha, uamuzi wa
kuanzishwa VMW ulitokana na Waraka wa Baraza la Mawaziri No. 96 wa mwaka 1974
ambapo vyuo 25 vilianzishwa mwaka 1975 na kuendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka
kulingana na jinsi Wilaya mbalimbali zilivyo tambua umuhimu wa kuanzisha vyuo
hivi. Hadi kufikia mwaka 1978, vyuo 53 vilikuwa vimeanzishwa.
Uanzishwaji wa VMW ulizingatiwa katika Sheria ya Elimu No.
25 ya mwaka 1978 chini ya Wizara ya Elimu. Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi
vilipoanzishwa vilirithi majengo yaliyokuwa yakitumika kwa madhumuni tofauti
tofauti vikiwemo Vituo vya Mafunzo ya Maendeleo Vijijini (Rural Training Centres) ambavyo vilianzishwa
mwaka 1962, Vituo vya Mafunzo ya Wakulima (Farmers Training Centres) ambavyo
vilianzishwa mwaka 1963, Shule za Kati (Middle Schools) ambazo
zilianzishwa mwaka 1960 na Vituo vya Mafunzo ya Ushirika vilivyoanzishwa mwaka
1964. Vyuo pekee vilivyojengwa mahsusi kuitikia wazo la Baba wa Taifa la mwaka
1975 ni vinne, vyuo hivyo ni Sengerema, Ngara, Handeni na Bigwa, ambavyo
vilijengwa mwaka 1975.
LENGO NA MADHUMUNI YA KUANZISHWA KWA VYUO VYA MAENDELEO YA
WANANCHI (VMW)
Lengo Kuu
Lengo kuu la kuanzisha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi lilikuwa
ni kuimarisha maarifa na stadi kwa wananchi ili waondokane na ujinga, umaskini
na maradhi na hatimaye kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na
kiutamaduni.
Madhumuni mahsusi yakuanzisha VMW
Madhumuni mahsusi ya vyuo hivi yameelezwa katika Waraka wa
Serikali Na. 96 wa mwaka 1974 ambapo kipengele cha 5 kinaainisha madhumuni
yafuatayo:
a) Kumtayarisha Mtanzania ambaye ni mtu mzima
aweze kukuza utu wake na kumfanya awe kamili katika jumuiya ya Watu wake;
b) Kumtayarisha Mtanzania aweze kutumia akili zake
vizuri na kuweza kuamua mambo yake au ya Umma kwa njia iliyo sahihi;
c) Kumsaidia Mtanzania aelewe siasa ya nchi yake
na kumwezesha kushiriki kikamilifu bila woga au unafiki katika shughuli za
siasa ya nchi yake;
d) Kujenga moyo wa Mtanzania wa kushirikiana
na wenzake katika shughuli au kazi za nchi yake, na kuelewa umuhimu wa
kuwa na uhusiano mwema na wenzake;
e) Kumwezesha Mtanzania aweze kufikia kiwango
cha juu zaidi katika ufundi wa kazi anazozifanya;
f) Kumsaidia Mtanzania kukuza utamaduni
wa Kitanzania; na
g) Kuwafanya Watanzania wawe raia wenye
manufaa katika Tanzania na dunia nzima.
Lengo na madhumuni haya yaliendelea kutekelezwa hadi mwaka 1987
ilipoundwa Tume ya Nsekela iliyoazinsha majukumu ya Wizara na Idara mbalimbali
za Serikali. Tume ya Nsekela ya Februari 1987 ilibaini kuwa madhumuni na
majukumu ya Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi yanashabihiana sana na yale ya
Maendeleo ya Jamii ya kuwajengea uwezo wananchi ili wamudu majukumu yao vyema
na kuboresha utendaji na maisha yao. Tume hiyo iliishauri Serikali kuhamishia
VMW katika Idara ya Maendeleo ya Jamii. Mwaka 1990, Serikali ilivihamishia
VMW katika Idara ya Maendeleo ya Jamii chini ya iliyokuwa Wizara ya Maendeleo
ya Jamii, Wanawake na Watoto. Ingawa lengo kuu halikubadilika, madhumuni
yaliboreshwa ili kukidhi mabadiliko ya wakati huo katika jamii kwa kuzingatia
Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025.
Madhumuni mahsusi yaliyoboreshwa
Madhumuni yaliyoboreshwa ni yafuatayo:
a) Kuwapatia wananchi stadi mbalimbali za
ujuzi na maarifa ambayo yatawasaidia kujiajiri na kuajiriwa hivyo kuondoa
umaskini katika jamii;
b) Kuwawezesha viongozi katika ngazi za Vijiji na
Kata kuelewa majukumu yao na hivyo kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa sera
mbalimbali za Serikali za kuondoa umaskini, kuwaletea wananchi maisha bora na
kusimamia misingi ya utawala bora;
c) Kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu
katika maamuzi, kutambua masuala ya jinsia, kuimarisha na kudumisha utamaduni
wa kupiga vita mila na desturi zinazomkandamiza mwanamke katika jamii;
d) Kuziwezesha jamii kuelewa umuhimu wa
hifadhi, matumizi bora ya mazingira na kutumia rasilimali zilizopo kwa faida
yao; na
e) Kuziwezesha jamii kuelewa na kujikinga na
janga la UKIMWI.
Majukumu ya Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi
Ili kufikia madhumuni tajwa hapo juu VMW vimepewa majukumu
mbalimbali kupitia “Mwongozo wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi” wa mwaka 2002.
Majukumu hayo ni pamoja na:
a) Kutoa mafunzo yenye kuongeza maarifa, stadi
na mbinu mbalimbali za kutatua matatizo halisi ya wananchi, ili wajiletee
maendeleo kwa kutumia rasilimali zilizopo;
b) Kutoa mafunzo yanayokidhi mahitaji halisi ya
wananchi na soko;
c) Kubuni na kuendesha miradi ya uzalishaji
mali na utoaji huduma vyuoni na kuvisaidia vijiji vinavyozunguka vyuo. Aidha,
miradi hii ifanyiwe uchambuzi na upembuzi yakinifu ili miradi inayotekelezwa
iwe na taathira chanya kwa jamii;
d) Kushirikiana na asasi na mashirika
mbalimbali yanayotoa mafunzo, utaalam na rasilimali nyinginezo kuwaendeleza
wananchi. Katika zoezi hili, vyuo vitapata fursa ya kubadilishana uzoefu
na asasi hizo;
e) Kufanya utafiti wa mahitaji utakaotoa
takwimu na taarifa sahihi zitakazotumiwa na vyuo, vijiji na mitaa, katika
kubuni, kupanga na kutoa mafunzo ya ushirikishwaji, pamoja na kutekeleza miradi
mbali mbali ya kujitegemea. Aidha taarifa na takwimu hizo zinaweza
kutumiwa na Halmashauri za wilaya, Miji, Manispaa na Jiji katika kuandaa
mipango ya uwiano ya maendeleo;
f) Kuwa vituo vya kufundishia,
kutengeneza na kusambaza teknolojia na nyenzo za kurahisisha kazi wafanyazo
wananchi;
g) Kubaini mila zisizo za maendeleo na vikwazo
vingine vya maendeleo katika maeneo vilipo vyuo na kutoa mafunzo dhidi ya
vikwazo na mila hizo;
h) Kubuni, kuandaa na kuendesha programu
mbalimbali zitakazoinua kiwango cha fikra, maarifa na stadi za wananchi
kuhusu mazingira yao na ulimwengu kwa jumla;
i) Kuendesha programu mbalimbali za
hifadhi ya mazingira kwa wananchi zinazohusu matumizi bora ya ardhi kwa
kuzingatia kanuni za kilimo na ufugaji bora, upandaji miti na maua na utunzaji
wa vyanzo vya maji;
j) Kuwashirikisha wananchi katika
mijadala inayohusu masuala ya jinsia;
k) Kubuni mikakati ya namna ya kuwafuatilia
wahitimu kwa nia ya kupima kiwango cha taathira kilichofikiwa kutokana na
mafunzo yanayotolewa vyuoni, matokeo ya upimaji huo yatatumika katika
kurekebisha mitaala na mikakati ya utekelezaji; na
l) Kushirikiana na asasi nyingine za
Serikali, madhehebu ya dini mbalimbali na Mashirika yasiyo ya Kiserikali na
Wananchi kubuni na kutekeleza programu na miradi madhubuti ya kutokomeza janga
la UKIMWI na umaskini na kupiga vita rushwa.
SERIKALI KUBORESHA VYUO VYA MAENDELEO
YA WANANCHI.
Serikali imesema kuwa itahakikisha inafanya maboresho katika
vyuo vyote vya Maendeleo ya Wananchi hapa Nchi ili kuondoa adha mbalimbali
zinazovikabili vyuo hivyo sambamba na kuondoa changamoto zinazowakabili
wanafunzi vyuoni ikiwemo ya uchakavu wa majengo na miundombinu.
Hayo yamesemwa Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya,
Maendeelo ya Jamii, Jinsia na Watoto Dkt. Hamisi Andrea Kigwangala wakati
akijibu swali la Mbunge wa Nanyamba Abdallah Chikota aliyetaka kujua Serikali
ina mpango gani wa kuboresha miundombinu na utoaji wa taaluma ya Chuo cha
Maendeleo ya Wananchi (MTAWANYA) kilichopo Mkoani Mtwara.
Akijibu swali hilo Dkt.Kigwangala amesema kuwa Serikali ina
mpango mkakati mpya wa kufanya maboresho katika vyuo vyote vya maendeleo ya
Wananchi hapa Nchini ambapo kwa kipindi hiki Wizara ipo katika mazungumzo na Wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi
ili kuweza kuvihamishia Kwenye Wizara hiyo ya elimu.
Aidha ameongeza kuwa lengo kuu la kufanya hivyo ni kuboresha mitaala inayotolewa katika vyuo
hivyo lakini pia kuboresha utawala wa vyuo na kuongeza bajeti.
“Tunafahamu
kero mbalimbali zinazovikabili vyuo vyetu vyote, tupo njiani kufanya baadhi ya
marekebisho ili kuweza kuondoa kero hizo kwa wahusika” Alisema Kigwangala.
No comments:
Post a Comment